- Mifugo

Wafahamu Nzi chuma (Black soldier Fly), protini mbadala ya mifugo

Sambaza chapisho hili

Nzi chuma (Black Soldier Fly), kwa kisayansi Hermetia illucens (Linnaeus) ni aina ya nzi katika kundi la Stratiomyidae ambao hupatikana sana katika ukanda wa Magharaibi mwa hemisphere yaani mabara ya Marekani ya kusini na kaskazini, sehemu ya Africa, Ulaya, Antactical, Asia na pia Australia.

Nzi hawa hawana madhara ya aina yoyote kwa binadamu kwa sababu hawana mfumo wa chakula mwilini mwao. Aidha, hawana midomo ya kuwawezesha kula chakula sawa na nzi wengine wa nyumbani na hivyo hawawezi kuuma. Nzi mzima moja ana wastani wa inchi 7/8 na nzi jike huwa na rangi ya uwekundu na miguu yao ni mieusi.

Nzi chuma ameleta mapinduzi makubwa sana ya wadudu wenye kutoa suluhu kwenye sekta ya chakula cha mifugo. Hii ni kwa sababu hawa wadudu wanaweza kukua kwenye aina yoyote ile ya taka hai, ikitoa kiwango cha juu cha protini cha hadi asilimia 44 na lipid ya asilimia 36.

Gharama za juu za vyakula vya mifugo hasa protini ni moja ya sababu ya watu kuanza kutafuta suluhisho la nafuu la chakula cha kulisha mifugo. Hii ni kwa sababu vyakula vya mifugo hasa protini vina ushindani kati ya binadamu na mifugo, kitu kinacho pelekea bei kuwa juu.

Faida za nzi hawa

  • Kupunguza upotevu wa vyakula
  • Kupunguza gharama za vyakula vya mifugo
  • Kuongeza virutubisho kwenye udongo.
  • Kuku wanaolishwa nzi chuma kama protini huongezeka uzito kwa asilimia 92 zaidi ya kuku watakao lishwa soya au protini nyingine.
  • Kwa kuku wa nyama, huongeza uwezo wa kuku kuhimili magonjwa kama taifod ya kuku ( Gallinarum). Nzi hawa pia wana kinga iitwayo prophylactic ambayo huchochea kinga kuwa imara kukabili magonjwa
  • Wana amino asidi bora kuliko iliyoko kwenye soya.
  • Pia kwa mujibu wa tafiti nzi chuma wana uwezo wa kuongeza ukuaji wa haraka wa kuku wa nyama.
  • Kwa kila kilo 1 ya uchafu inayoliwa na funza basi hupatikana protini gram 50
  • Kwa mwaka heka 1 ya nzi chuma inaweza kuzalisha protini nyingi sana kuliko heka 3000 za ng’ombe au heka 130 za soya.

Nzi chuma wanaweza kutengeneza Funza kwa ajili ya Mifugo

Mifugo mingi inaweza kutumia funza watokanao na nzi chuma kwa chakula.

  • Aina zote za ndege kama vile kuku wa aina zote, kanga, bata, kware wanaweza kulishwa hawa funza kwa asilimia 100 na wasipewe chakula kingine chochote kile.
  • Samaki wa aina zote pia wanaweza kulishwa funza hawa kama chakula.
  • Ng’ombe wa maziwa na hata wa nyama.
  • Nguruwe, mbwa pamoja na paka.

Uzalishaji wa funza kutokana na nzi chuma

Funza ndicho chakula kinachotumika kulisha mifugo, na funza hawa wanazalishwa au wanatokana na nzi chuma.

Ili uweze kuzalisha hawa funza watokanao na nzi chuma inakubidi kuwa na vitu vifuatavyo;

  • Banda la kutunzia nzi chuma. Banda hili hujengwa kwa kutumia neti maalumu na laweza kukaa tu nje na likawa wazi ila nzi lazima wawe ndani ya neti.
  • Banda la kutunzia funza. Funza hawapatani na jua hivyo ni lazima wajengewe banda lao wenyewe na lisiruhusu mwanga wa jua kuingia ndani.
  • Vyombo vya kuwatunzia funza. Unaweza kutumia mabeseni au ukajenga karo ambalo utakuwa unawalishia humo.

Jinsi ya kupata hawa funza ili kuzalisha

Ili upate funza ni lazima uwe na mayai ya nzi chuma na ili upate mayai hayo ni lazima kuwa na hao nzi chuma. Hivyo njia ya kuwapata ni kwa kuwatega hawa nzi chuma ili waje watage mayai na mwishowe uangulishe mayai kupata funza.

Njia nyingine ni kwa kununua funza hai kutoka kwa wazalishaji na baadaye funza hao kubadilika na kuwa nzi kisha kutaga mayai na baadaye funza tena.

Chakula cha hawa funza

Aina zote za taka hai yafaa kwa ajili ya kulishia funza. Taka hai ni taka zinazo oza au ambazo zilikuwa na uhai mwanzo yaani mabaki yote ya vyakula, mizoga ya aina zote, majani na kadhalika.

Taka hai unaweza kuzipata majumbani au kwenye masoko ambako ndo hasa kunazalishwa taka hai kwa wingi.

Maisha ya hawa funza

Nzi chuma wana maisha mafupi sana ya siku 7 tu ila ndani ya hizo siku 7 hawa nzi wanakuwa wameisha taga mayai ambayo hayo mayai huangulika baada ya siku 4 na baada ya hapo utapata funza.

Funza watakula chakula kwa muda wa siku 14 na baada ya hapo watakuwa wamefikia kuvunwa kulishia mifugo. Baada ya siku 14 kama hujawavunwa kulishia mifugo basi hawa funza huanza kuabadilika na kuwa buu ambaye huduma kwa siku 14 zingine kabla ya kurudi kuwa nzi tena.

Usalama wa hawa nzi chuma na funza

Nzi chuma hawa ni salama kwa asilimia 100 kwa saababu zifuatazo;

  • Nzi Chuma hawa hawali chakula kama ilivyo kwa nzi wa majumbani hivyo ni vigumu sana kwa hawa inzi chuma kueneza magonjwa. Nzi chuma huishi kwa mvuke wa maji pekee kwa hizo siku 7.
  • Funza mbali na kutupatia protini pia hutumika kupambana na bakteria na fangasi, hakuna bakteria na fangasi anaye weza kuishi sehemu ambayo kuna hawa funza.

Hivyo hawa funza ni salama na unaweza kuwazalishia nyumbani kwako na hata ukatenganisha vyumba vingine ukaishi na vingine ukazalishia hawa funza.

Virutubisho vinavyopatikana kwenye funza

Sababu kuu ya kugeukia uzalishaji wa funza watokanao na nzi chuma ni kwa sababu ya virutubisho vinavyo patikana kwenye na kuleta mbadala kamili wa soya, dagaa na Samaki.

Funza wana virutubisho vifuatavyo;

Protini, Lysine, Arginine, Methionine, Leucine, Threonine, Mafuta, kalisi, majivu, nyuzinyuzi, Dry Matter, Metabolism energy.

Kiwango cha protini kwenye funza ni kuanzia asilimia 50 na kuendelea na huweza kufika hadi asilimia 60. Ili kujua kiwango cha protini unaweza kupima kwenye maabara ya taifa ya mifugo iliyoko Dar es salaam.

Kwa mawasiliano zaidi, wasiliana  Charles Shauri  kutoka Go-Insects Arusha, Kisongo. Barua pepe cshauri@gmail.com Simu +255767691071

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

2 maoni juu ya “Wafahamu Nzi chuma (Black soldier Fly), protini mbadala ya mifugo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *