- Mifugo
Sambaza chapisho hili

Kabla hujaamua kufuga sungura hakikisha ya kwamba umejitoa na unamuda wa kuwahudumia wanyama hawa. Ufugaji wa sungura si rahisi kama vile ukifuga paka au mbwa.

Sungura wanahitaji uangalizi hasa kwenye usafi kwa sababu ni rahisi kwao kupata maradhi yatokanayo na mazingira mabaya na machafu.

Mabanda

Kuna aina mbili ya mabanda ya kufugia:

  • Kwanza ni mabanda ya kufugia ndani muda wote bila kutoka nje.
  • Pili ni ile nusu nusu, yaani sungura wanakua na mabanda na wanaweza kutoka nje kwenye ua maalum.

Katika aina zote hizi mbili ni muhimu kuhakikisha hakuna upenyo wa kuruhusu panya kupita kwasababu, panya huwa wanakula watoto wa sungura.

 

 

 

Ufugaji wa ndani

  • Usitumie banda la kioo (aquarium) kwa sababu halina hewa ya kutosha na ni vigumu kusafisha.
  • Sakafu ya nyavu za waya ni nzuri zaidi, ila hakikisha hakuna sehemu zenye ncha kali inayoweza kuwaumiza sungura. Sungura wakiumia ni mpaka wapone wenyewe au achinjwe kwa sababu ukitumia dawa za antibiotic sungura hana uwezo wa kuzimeng’enya na kuisha mwilini mwake.
  • Ukubwa wa banda usipungue mita 4×2 kwa kila sungura mmoja, likiwa kubwa zaidi ni vizuri.
  • Chini kuwekewe matandazo kama nyasi kavu au maranda ya mbao.
  • Maranda yatokanayo na miti yenye mafuta kama mi-pine na mikaratusi hayafai.
  • Wawekee Sungura kipande cha blanket au taulo la zamani kwa ajili ya kulalia na kuzalia hasa kwa wazazi.
  • Ni muhimu kuwawekea sehemu ya kujificha mara wanapohisi hatari, unaweza kutumia mbao, boksi gumu au plastiki.

Ufugaji wa nje

  • Sehemu yote izungushiwe wavu wa kuku kuzuia panya kuingia na wanyama wengine kama paka, mbwa, mwewe na wengineo wanaodhuru sungura.
  • Upande mmoja uwe na mabanda, sehemu ya chakula na maji pamoja na kivuli kwa ajili ya sungura kupumzika.
  • Futi moja chini ya udongo kuwe na zege kuzuia sungura kuchimba na kwenda mbali.
  • Eneo lijengewe mazingira ya kutokuwa na hatari zozote za sumu kama dawa za kuulia wadudu au mbolea.
  • Majani yaliyoota yasiwe yenye sumu (waone wataalamu wakushauri au ng’oa yote).

Utunzaji na ulishaji wa Sungura

Maji

Tumia bakuli ya kigae, plastiki au jenga kwa saruji. Maji yabadilishwe kila siku na vyombo visafishwe kila siku.

Chakula

Sungura wapewe majani, mabaki ya mboga za jikoni baada ya kuchambuliwa. Unaweza kuwawekea pumba au chakula cha kuku (growers mash) kwenye vyombo maalum kama chakula chenye virutubisho (concentrates).

Usafi

Kila siku jaribu kuondoa uchafu kama vyakula vilivyomwagika, na kinyesi kilichoganda kwenye matandazo, fagia na kubadili matandazo angalau mara moja kwa wiki. Manyoya ya sungura mzani yasiondolewe, hii huonesha kwamba anakaribia kuzaa.

Meno

Wakati mwingine meno ya mbele hukua sana na kumsababishia usumbufu sungura wakati wa kula, waone wataalamu ukiona yamerefuka zaidi na yanahitaji kupunguzwa. Dalili kuu ni sungura kushindwa kula kwa zaidi ya saa 12.

Miguu

Miguu ya sungura si kama ya wanyama wengine, nyayo zake zimefunikwa kwa manyoya, angalia ukiona yananyonyoka kuna tatizo chunguza, kucha zake nazo huhitaji kupunguzwa zikikua sana.

Ubebaji

Usimbebe kwa kutumia masikio yake huwa wanaumia sana, shika ngozi nyuma ya shingo kama paka ukitaka kumbeba

Dawa

Wapewe dawa ya minyoo kama vile piperazine kila baada ya miezi mitatu, dawa za wadudu kama akheri powder zinyunyiziwe kwenye mabanda yao kuzuia viroboto, usiwape dawa nyingine bila ushauri wa kitaalamu.

Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana na mtaalamu wa mifugo kutoka SUA Augustino Chengula kwa simu +255 676 605 098

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *