- Mimea

Namna bora ya kuvuna na kusindika mbaazi

Sambaza chapisho hili

Nimelima zao la mbaazi kwa muda mrefu sana, na miaka yote nimekuwa nikipata faida, mpaka hivi karibuni bei ya zao hili ilipoanguka na tukapata hasara. Je ni namna gani naweza kuhifadhi zao hili au kusindika? Msomaji MkM-Arusha.

Mbaazi ni kati ya mazao jamii ya mikunde ambayo hulimwa kwa wingi katika mikoa ya Mtwara, Dodoma, Lindi, Pwani, Morogoro, Arusha, Manyara, Tanga na Kilimanjaro. Maandalizi kabla ya kuvuna Katika maandalizi ya uvunaji, mkulima hana budi kuzingatia mambo yafuatayo.

Kukagua shamba

Kagua shamba kuona kama mbaazi zimekomaa. Mbaazi hukomaa kati ya miezi minne hadi miezi tisa kutoka kupandwa kutegemeana na aina. Wakati huo unyevu wa punje huwa kati ya asilimia 20 na 25. Mapodo hubadilika rangi kutoka kijani na kuwa ya kahawia. Aandaa vifaa au vyombo vya kuvunia. Vifaa hivyo ni mapanga, maturubai, mifuko, vyombo vya usafirishaji, sehemu ya kukaushia na ya kupuria na ghala.

Kuvuna

Kwa kawaida mbaazi huvunwa kwa mikono. Mbaazi zilizokomaa huvunwa kwanza kwa kuchuma mapodo au kukata matawi na kuacha zilizo changa ziendelee kukomaa. (Vuna kila baada ya siku tatu hadi tano). Ni muhimu kuvuna mapema ili kuepuka upotevu unaosababishwa na kupasuka kwa mapodo pamoja na mashambulizi ya wadudu

Kusafirisha

Mbaazi zilizovunwa husafirishwa kutoka shambani hadi nyumbani kwa kutumia njia mbalimbali kama vile kubeba kichwani,toroli na baiskeli. Pia kwa kutumia wanyama kama punda, mikokoteni ya mikono, mikokoteni ya wanyamakazi, matela ya kuvutwa na trekta na magari.

Kukausha

Hatua ya kwanza ni kukausha mapodo ili kurahisisha upuraji na hufanyika mara baada ya kuvuna. Mapodo hukaushwa kwenye kichanja bora, maturubai au sakafu safi.

Kupura

Upuraji wa mapodo hufanyika baada ya ukaushaji wa awali kwa kutumia mikono. Mapodo huwekwa kwenye magunia, hutandazwa sakafuni au kwenye maturubai. Pigapiga kwa kutumia mti hadi mapodo yote yapasuke na punje zote zimeachia. Ukaushaji huu hufanywa mara baada ya kupura ili kupunguza unyevu kwenye punje hadi kufikia asilimia kati ya 20 na 25.

Kupepeta na Kupembua

Kazi ya kupepeta na kupembua hufanywa kwa mikono ambapo ungo au beseni hutumika. Takataka nyepesi hupeperushwa na upepo wakati zile nzito huondolewa kwa kutumia mikono (Chekeche pia huweza kutumika).

Kupanga madaraja

Baada ya kupepeta na kupembua, punje za mbaazi hupangwa kwenye madaraja kulinga na aina, rangi na ukubwa. Daraja la juu lina sifa ambazo ni punje zisiwe zimeshambuliwa na wadudu au magonjwa, ziwe na rangi moja, na ziwe na ukubwa mmoja.

Kufungasha na Kuhifadhi

Baada ya kupepeta na kupembua fungasha mbaazi kwenye magunia safi na hifadhi kwenye ghala bora na safi. Inapobidi changanya mbaazi na kiuwadudu aina ya Actellic Super Dust kwa kiwango cha gramu 100 kwa kilo 100 za mbaazi.

Usindikaji wa Mbaazi

Punje za mbaazi mbichi hutumika kama mboga na hakuna sababu ya kukoboa. Punje Kavu za mbaazi huwa na ganda gumu ambalo ni vigumu kuiva wakati wa kupika na pia husababisha ladha ya mbaazi kuwa ya uchungu. Mbaazi hukobolewa ili kuondoa ganda hilo na kurahisisha Mavuno bora ya mbaazi mkulima hupata kwa kuzingatia kilimo bora upishi.

Kukoboa punje kavu za mbaazi

Koboa punje kwa kutumia kiuri, kutumia jiwe aina ya chakki, au kwa kutumia mashine kubwa zinazoendeshwa kwa umeme.

Jinsi ya kukoboa

Chagua mbaazi safi na zilowekwe kwa saa 8 hadi 14 kisha kausha punje za

mbaazi juani kwa siku tano hadi sita. Koboa na paraza (splitting) mbaazi kwa kutumia jiwe maalumu (Chakki) kwa kuweka mbaazi kavu katikati ya vipande viwili vya mawe na kuzungusha jiwe na huku ukibonyeza kwa kutumia nyenzo.

Kama jiwe la kukoboa mbaazi halitakuwepo basi unaweza kukoboa kwa kutumia kinu. Peta na chagua punji zisizokobolewa ili zirudiwe tena kukobolewa, kwa kuzichemsha tena kwa dakika15, kukausha na kukoboa kama ilivyoelezwa. Aidha unaweza kuzikaanga kwa dakika tatu hadi tano na zikishapoa unakoboa kama hapo juu. Mbaazi zilizokobolewa hazishambuliwi na wadudu kwa urahisi na hifadhi yake huchukua muda mrefu bila kuharibika.

Matumizi

Hutumika katika mapishi mbali mbali kama vile utengenezaji wa supu, bongko na aina mbali mbali za mseto. Kwa maelezo zaidi kuhusiana na makala hii wasiliana na Afisa Kilimo kutoka halmashauri ya Arusdha, Bi.Lucy Mvungu kwa simu +255 755 565 621 Makala hii imeandaliwa na Shirika la Kilimo Endelevu Tanzania

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *