- Mifugo
Sambaza chapisho hili

Homa ya nguruwe ni ugonjwa hatari wa nguruwe unaosababishwa na virusi aina ya African Swine Fever vinavyoshambulia na kuharibu mfumo wa damu. Virusi vinavyosababisha homa ya nguruwe haviambukizi binadamu.

Virusi vinavyosababisha homa ya nguruwe huishi kwenye miili ya ngiri bila kusababisha ugonjwa.

Kupe laini walioko katika mashimo wanamoishi ngiri, hupata virusi vya homa ya nguruwe wanaponyonya damu kutoka kwa ngiri walioathiriwa na virusi. Virusi hivi vya homa ya nguruwe huzaliana katika kupe hawa laini.

Ngiri hudondosha kupe wenye virusi vya homa ya nguruwe kwenye mabanda ya nguruwe wakati wanapoenda usiku kutafuta chakula katika makazi ya binadamu. Kupe humfikia nguruwe na kisha huambukiza virusi kwa nguruwe wakati wanaponyonya damu. Nguruwe wanapoambukizwa virusi hupatwa na homa kali na karibia nguruwe wote hufa katika kipindi kifupi tangu ugonjwa unapoingia katika banda.

Kuanzia hapa, ugonjwa huu husambaa kutoka nguruwe walioathirika kwenda kwa nguruwe ambao hawajaathirika.

Uchinjaji holela wa nguruwe wanaoumwa husababisha virusi kusambaa kwenda kwa nguruwe ambao hawaumwi kwa kulisha mabaki ya nguruwe walioathirika, kushika damu yenye virusi na kisha kwenda kulisha nguruwe, kukanyaga damu yenye virusi machinjioni na kisha kwenda na viatu hivyo kwenye mabanda ya nguruwe ambao hawajaathirika.

Dalili za ugonjwa wa nguruwe

  • Nguruwe hunyong’onyea na kukosa hamu ya kula na kukusanyika mahali pamoja.
  • Joto la mwili huongezeka hadi nyuzi 42°C kutoka 38.7°C -39.8°C za kawaida.
  • Nguruwe huwa na rangi ya ubluu au nyekundu katika sehemu za mwili hasa zisizo na manyoya marefu kwenye masikio, nyuma ya mapaja na chini ya tumbo na miguu.
  • Kutoa kinyesi chenye damu na wakati mwingine kushindwa kusisimama.
  • Kutapika na kuharisha, hupungua uzito.
  • Kutupa mimba na vifo hutokea baada ya wiki moja hadi mbili.
  • Ukipasua ndani utakuta kongosho, figo na viungo vingine vikiwa vimevimba na kujaa damu.

Kudhibiti ugonjwa wa homa ya nguruwe

Uzuiaji na utokomezwaji wa ugonjwa wa homa ya nguruwe unategemea sana ushiriki wa wafugaji na jamii ili kuongeza uelewa wa njia zinazozuia virusi visifike katika nguruwe wanaowafuga kutoka kwa ngiri au uambukizwaji kutoka kwa nguruwe wagonjwa kwenda kwa nguruwe wasio na ugonjwa wakati wa mlipuko.

 

 

Hatua zifuatazo zinaweza kutumika kudhibiti ugonjwa

  • Jenga banda la kufugia nguruwe kulingana na ushauri wa mtaalamu wa mifugo. Usitumuie ufugaji huria (kuchunga). 3
  • Tengeneza sehemu ya kuweka dawa ya kukanyga wakati unaingia na kutoka kwenye banda.
  • Kuepuka kusafirisha nguruwe na mazao yake kwenye wilaya zilizoathirika na ugonjwa.
  • Kutokununua nguruwe au mazao yao kutoka katika maeneo yaliyoathirika kwa kushawishika na kushuka kwa bei.
  • Wafugaji wasiruhusu wachinjaji au wafanyabiashara kuingia katika mabanda na kuchagua nguruwe wa kununua.
  • Wafugaji waepuke kulisha nguruwe mabaki ya nguruwe wanayokusanya kutoka mahotelini au katika vituo kunakoandaliwa na kuliwa nyama ya nguruwe.
  • Chakula cha nguruwe lazima kitoke katika maeneo ambayo hayana Ugonjwa.
  • Watu tofauti na mhudumu wasikaribie au kuingia katika banda la nguruwe.
  • Wafugaji wapulizie dawa za kuua virusi na kupe kwenye mabanda na nguruwe ili kudhibiti vimelea vya ugonjwa.
  • Waepuke kuchanganya nguruwe wageni na wenyeji kwenye banda moja.
  • Wafugaji wahakikishe wanatoa taarifa za ugonjwa au vifo vya nguruwe mara vinapotokea kwa mtaalamu wa mifugo aliye karibu.
  • Nguruwe waliokufa kwa ugonjwa wa homa ya nguruwe wafukiwe kwenye shimo refu au wateketezwe kwa moto.

 

Kwa mawasiliano zaidi wasiliana na Prosper Linus, afisa mifugo, wilaya ya Arumeru Arusha kwa simu namba 0756663247

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *