Mipango thabiti huleta mafanikio katika ufugaji
July 5th, 2013
<< rudi


Mipango thabiti huleta mafanikio katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa. Wafugaji waliofanikiwa wanafahamu fika kuwa katika uzalishaji wa maziwa 20% inatokana na aina ya ng’ombe na 80% matunzo.


Tumekutana na kupokea maombi kutoka kwa watu wengi ambao wanataka kuanzisha ufugaji wa ng’ombe, lakini hawajui ni wapi pa kuanzia. Kwa kawaida, wao wanaweka pesa, kutafuta ng’ombe, kununua na mwisho hupata ng’ombe. Hapo ndipo kuhangaika na kupata msongo wa mawazo kwa mfugaji huanza kwa kuwa ng’ombe hazalishi maziwa kutokana na aina yake pekee.


Kwa wafugaji wadogo walio wengi, wakati ambapo ng’ombe anafika zizini kwake wanakuwa bado hawajawa tayari kumpokea ng’ombe huyo kwa ajili ya ufugaji. Ili ujasiria mali kwa njia ya ng’ombe uweze kufanikiwa na kumfaidisha mfugaji kiuchumi, mfugaji ni lazima ahakikishe kuwa miundo mbinu muhimu inakuwa tayari kabla ya kumleta ng’ombe.


Kwa mujibu wa mwongozi wa kitabu cha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa Afrika ya mashariki, ng’ombe wa maziwa ni lazima wapate mahitaji yafuatayo:

• Malisho bora na maji safi ya kunywa

• Afya bora bila majeraha

• Mazingira safi ikiwa ni pamoja na  banda lililojengwa vizuri

• Uangalizi mzuri na wa kirafiki,  ambao humfanya ng’ombe kuwa mtulivu bila kuwa na msongo.


Bila mahitaji haya muhimu, na mfugaji kutokumtunza ng’ombe vizuri, asitegemee kuwa ng’ombe huyo atazalisha kiwango kizuri cha maziwa. Uzalishaji wa kiwango cha maziwa na ubora wake unategemeana kwa kiasi kikubwa na mambo hayo yaliyotajwa hapo juu. Wataalamu wanasema kuwa 20% ya uzalishaji wa ng’ombe inatokana na aina ya ng’ombe na 80% matunzo kutoka kwa mfugaji. Muhudumie ng’ombe wako vizuri naye atarudisha kwa kuzalisha maziwa vizuri.


Mipango


Wafugaji ni lazima wawe na mipango thabiti kwa ajili ya ufugaji wa ng’ombe. Hii hujumuisha idadi ya ng’ombe mfugaji anayotaka kufuga, pamoja na kufahamu ni kiasi gani cha malisho kinachohitajika kwa kipindi chote cha mwaka. Mfugaji pia anapaswa kufahamu kuwa ni kwa namna gani malisho yanafaa kutolewa kwa wanyama.


Mfugaji ni lazima pia apange ni kwa namna gani atapata malisho kwa kipindi chote. Hii inamaanisha kuwa ni muda gani atapanda, kuvuna na kuhifadhi. Mipango ni nguzo muhimu sana kwa kuwa inawezesha kusaidia kufahamu ni nini cha kufanya, namna ya kufikia malengo yaliyokusudiwa, na ni hatua gani imefikiwa. Mfugaji ambaye hana mipango thabiti ni sawa na mtu anayeanza safari bila kufahamu mwisho wa safari yake ni wapi.


Mahitaji ya mlo kamili


Shughuli ya ufugaji wako itakamalika siku ambayo utaweza kuelewa uhusiano kati ya ulishaji wa ng’ombe, uzalishaji wa maziwa na mapato. Endapo ng’ombe wa maziwa atalishwa kwa malisho hafifu ni dhahiri kuwa uzalishaji wa maziwa pia utakuwa hafifu.


Malisho bora


Tafuta ni aina gani ya malisho hufanya vizuri katika ukanda wako. Malisho endelevu hutegemeana kwa kiasi kikubwa na aina ya malisho na utunzaji wake shambani mwako. Chukulia kuwa wewe ni mfugaji mdogo na hauwezi kumudu gharama za umwagiliaji, ni lazima utumie kwa kiasi kikubwa malisho ya wakati wa mvua na kuhifadhi ili kuweza kuyatumia wakati wa kiangazi.


Inashauriwa kupanda majani ya malisho kwa kiasi kikubwa uwezavyo wakati wa mvua. Wahamasishe majirani zako kupanda malisho pia, ili baadaye uweze kununua kutoka kwao. Matete, nyasi, majani ya mtama, majani ya mahindi, lusina, desmodiamu, na alizeti ni miongoni mwa malisho ambayo hufanya vizuri katika maeneo mengi nchini Tanzania.


Kiwango cha kutosha


Fahamu ni kiwango gani kinachotosha kwa kila ng’ombe wako. Hii itakusaidia kufahamu ni kiasi gani cha malisho upande na ni kiasi gani uhifadhi. Kwa wastani, ngombe wa maziwa aliyekomaa mwenye uzito wa kilo 400, anayefugwa ndani ana uwezo wa kula kilo 12 za majani makavu kwa siku. Kumbuka kuwa endapo mifugo yako haitapata malisho ya kutosha wataonesha kwa muonekana wao, na kisha kukupa adhabu kwa kuzalisha maziwa kidogo sana. Kama kanuni inavyoeleza, hakikisha kuwa 15%-18% ya malisho yote ni protini.


Zingatia utunzaji na uzalishaji wa malisho vizuri


Wafugaji walio wengi hukwepa kupanda majani ya malisho kwa kuogopa gharama ya mbolea na mbegu. Kwa uzoefu wetu mfugaji anaweza kutumia mbolea inayotokana na wanyama kupanda malisho na kuyatunza vizuri. Matete ni moja wapo ya malisho hayo. Endapo malisho hayo yatawekwa mbolea vizuri, shamba dogo tu la malisho linaweza kukupatia malisho ya mifugo kwa kipindi chote cha mwaka.


Weka malisho katika hali ya usafi


Hifadhi malisho katika sehemu nzuri, sehemu ambayo hayatapigwa na jua moja kwa moja, mvua au kuwepo uwezekano wa vitu vingine vinavyoweza kuyaharibu kama vile siafu na wadudu wengineo. Majani ya malisho ni lazima yanyaushwe vizuri kuepuka viini vya sumu vinavyoweza kuwepo kwenye malisho. Mfugaji anaweza kuamua juu ya ubora wa malisho kutokana na muonekano wake, harufu na mguso. Malisho mabichi yenye wingi wa majani kuliko shina, yenye kijani kilichokolea, na ambayo yana mguso nyororo, ni moja ya malisho bora ukilinganisha na yale yenye ugumu, shina kubwa na rangi ya njano. Epuka kulisha mifugo yako kwa kutumia malisho yenye ukungu kwa kuwa yanaweza kuwa na sumu.


Kuweka kumbukumbu ni muhimu


Uwekaji wa kumbukumbu ni muhimu lakini huwa hauzingatiwi na wafugaji walio wengi. Baadhi ya wafugaji huona kama uwekaji wa kumbukumbu ni kazi ya ziada, ambayo kulingana na wao haina uhusiano wowote na mapato yanayotokana na shughuli zao. Hata hivyo, bila uwekaji sahihi wa kumbukumbu, mfugaji hawezi kufahamu ni mapato kiasi gani anayopata kutokana na shughuli ya ufugaji. Ni kwa namna gani mfugaji anaweza kufahamu wakati wa kumpandisha ng’ombe wake, kama hajui kuwa zimepita siku ngapi tangu ng’ombe huyo alipozaa!


Alizeti ni chanzo cha malisho ya mifugo
March 27th, 2013
<< rudi


Alizeti haitoi mailisho pekee, pia inatoa mafuta bora kwa afya ya binadamu na pia malighafi inayotumiwa na nyuki kutengeneza asali.


Unapotengeneza chakula cha mifugo peke yako, si tu kupunguza gharama, lakini pia inakupa uhakika wa kuwa na chakula bora. Pia Wafugaji wa nyuki wanaopanda alizeti wanapata faida ya ziada kwa kupata asali iliyo bora kwa sababu nyuki hukusanya poleni kutoka kwenye alizeti wanapofanya ushavushaji.


Chanzo kizuri cha protini


Chakula cha mifugo kinachotengenezwa kutokana na alizeti ni chanzo kizuri cha protini kwa ajili ya mifugo, hasa ng’ombe wa maziwa, kuku, nguruwe na hata sungura. Malisho haya yana kiasi kikubwa cha protini, nyuzi nyuzi na kiasi kikubwa cha mafuta. Malisho haya yana protini kiasi cha asilimia 29-30, kiasi cha nyuzi nyuzi asilimia 27-31.


Moja ya tabia nzuri ya alizeti ni kwamba haina vitu vinavyoathiri virutubisho kwa mifugo, hata hivyo, ina kiasi kikubwa cha nyuzi nyuzi na mashudu yake kuwa magumu kiasi, jambo ambalo husababisha ugumu kidogo kwenye kusagwa tumboni. Mbali na virutubisho vya aina nyingine, alizeti ni chanzo kizuri cha kalishamu, fosiforasi na vitamini B.


Ubora wa alizeti inayotumika kwa ajili ya malisho ya mifugo inategemeana na namna ambayo imetayarishwa. Kwa mfano, alizeti inayosagwa bila kuondoa maganda ya nje, ina kiasi kikubwa cha nyuzi nyuzi (kati ya asilimia 27-30, lakini inakuwa na kiasi kidogo cha protini asilimia 23). Alizeti ambayo imetayarishwa kwa ubora wa hali ya juu huwa maganda yameondolewa na inakuwa na kiasi kikubwa cha protini, kiasi cha asilimia 40.


Mkulima anapaswa kufahamu kuwa alizeti bado inakuwa na virutubisho hata kama haitatayarishwa kwa ustadi. Mfugaji anaweza kutumia soya na karanga badala ya alizeti, lakini ni lazima apeleke alizeti kupima kuhakikisha kuwa ina nyuzinyuzi na virutubisho kwa kiwango cha nyuzinyuzi na protini kinachokubalika.


Inapendekezwa kutumia alizeti


Kulingana na utafiti ambao umefanyika nchini Tanzania, alizeti iliyochanganywa na pumba ya mahindi kwa kiasi cha asilimia 30, kisha kulishwa ng’ombe aina ya Zebu ina uwezo wa kuongeza uzalishaji wa maziwa kutoka lita 6.6 kwa siku mpaka lita 8.1 kwa siku. Nchini Zimbabwe, mashudu ya alizetu huchanganywa na mahindi pamoja na  mabua ya mahindi ambayo yamewekwa urea kwa kiwango cha wastani wa kilo 4.4 kwa siku, na kulishwa ng’ombe aina ya Jersey pamoja na ng’ombe chotara ambao hulishwa katika machungo ya wazi, Ng’ombe hawa huongeza kiasi cha maziwa kwa wastani wa kilo 5.8 mpaka kilo 6 kwa siku.


Aina ya alizeti


Kuna aina mbili za alizeti, alizeti fupi na alizeti ndefu. Aina ndefu hurefuka mpaka kufikia kiasi cha urefu wa mita 1.5-2.4. Uzalishaji wake ni hafifu ukilinganisha na mbegu za kisasa. Aina hii mara nyingi huwa ile inayojulikana kama Hungary nyeupe na Fedha. Alizeti fupi ni inayotokana na mbegu za kisasa ambayo huwa na urefu wa mita 1.2, aina hii huwa na mavuno mazuri zaidi ukilinganisha na aina ndefu.


Kutengeneza chakula cha mifugo


Kilo tatu na nusu za alizeti inapokamuliwa hutoa mafuta lita moja na mashudu kilo mbili na nusu.


Resheni kwa ng’ombe wa maziwa


•Changanya kilo 18 za mashudu ya alizeti na kilo 100 za pumba ya mahindi ili kutengeneza chakula cha ng’ombe.

•Mlishe ng’ombe anaezalisha maziwa kwa wingi kiasi cha kilo 4 ya mchanganyiko huo na kilo 2 kwa ng’ombe anaezalisha kiasi kidogo cha maziwa.

•Mbali na kulisha mchanganyiko huo, ng’ombe wa maziwa ni lazima apewe kiasi kingine cha chakula cha kawaida cha kila siku kama vile matete, hay, au aina nyingine yoyote ya malisho bora kwa kiasi cha kutosha.


Resheni kwa ajili ya kuku


Chakula cha kuanzia: Changanya kilo 22 za mashudu ya alizeti na kilo 100 za pumba ya mahindi Chakula cha kukuzia: Changanya kilo 20 za mashudu ya alizeti na kilo 100 za pumba ya mahindi au chenga.

Chakula kwa ajili ya kuku wanaotaga: Changanya kilo 18 za mashudu ya alizeti na kilo 100 za chenga za mahindi


ZINGATIA: Unapotengeneza chakula kwa ajili ya ng’ombe wa maziwa, mfugaji ni lazima ahakikishe kuwa mashudu hayazidi asilimia 20 ya resheni ya kulishia. Kwa ajili ya kulishia kuku, alizeti isizidi asilimia 7 ya jumla ya resheni.


Namna ya kuzalisha alizeti


Hali ya hewa: Alizeti hustawi vizuri zaidi kwenye udongo tifutifu, wenye rutuba ya kutosha. Zao hili lina mizizi inayoenda chini kwa kiwango cha kikubwa hivyo kuiwezesha kustawi hata katika sehemu yenye kiwango kidogo cha mvua. Kiasi cha wastani wa milimita 500-750 za mvua zinatosha kabisa kwa uzalishaji wa alizeti. Inaweza kulimwa kutoka usawa wabahari mpaka kufikia mwinuko wa mita 2600 kutoka usawa wa bahari.


Maandalizi ya shamba


Ni lazima kuhakikisha kuwa shamba limelimwa vizuri, ili kuweza kupata sehemu nzuri ya kusia mbegu.

Nafasi: Mbegu zinaweza kupandwa kwa nafasi ya sentimita 75 kwa 30 kwa kiasi cha kilo 2 kwa ekari moja (sawa na kilo 5 kwa hekari). Panda mbegu 3 kwa kila shimo, kisha acha mmea mmoja kwa kila shimo mimea inapofikia urefu wa sentimita 10-20.


Matumizi ya Mbolea


Alizeti hufanya vizuri kwenye udongo wenye rutuba. Matumizi ya mbolea inayotokana na miamba aina ya fosifeti inafaa zaidi kwa kuwa alizeti inahitaji fosifeti kwa kiasi kikubwa. Matumizi ya mbolea mboji iliyoandaliwa vizuri itaongeza virutubisho vya ziada kwenye udongo.

Alizeti hukua vizuri katika sehemu isiyokuwa na magugu. Palilia alizeti inapokuwa na urefu wa mita 0.7 (Kiasi cha wiki 4).


Ndege waharibifu


Ndege wanaweza kuharibu kiasi cha asilimia 50 ya alizeti endapo hawatafukuzwa. Ili kuzuia uharibifu huo, mkulima anaweza kuchukua hatua zifuatazo;

•Vunja shina la alizeti kufikia usawa wa magoti kabla ya alizeti kukauka. Unaweza pia kuvunja katika urefu wowote lakini alizeti iangalie chini ili kuzui ndege kudonoa.

• Ondoa alizeti shambani baada ya kukauka na kuihifadhi.

Ubanguaji unaweza kufanyikia nyumbani kwa kutumia fimbo

Alizeti ni lazima ikaushwe mpaka kufikia kiwango cha unyevu wa asilimia 10 kabla ya kuhifadhiwa


Ni rahisi kutunza kuku wa kienyeji
January 22nd, 2013
<< rudi


Unaweza kutunza kuku wa kienyeji na ukawa na kipato cha uhakika, pamoja na lishe nzuri kwa ajili ya familia.


Ulishaji: Kuku wa kienyeji wanaweza kulishwa kwa kumia mahindi, mchele, na mabaki ya ugali. Vyakula hivi ni lazima vikaushwe vizuri na kusagwa vizuri. Ulishaji ni lazima ufanyike katika sehemu safi au kwa kutumia vyombo vilivyotengenezwa maalumu kwa ajilii ya kulishia kuku.


Banda: Kuku wawe wa kienyeji au wa kisasa, wanahitaji kuwa na banda zuri kwa ajili ya malazi na kuwalinda. Wanahitaji chumba chenye nafasi ya kutosha na kinachopitisha hewa ya kutosha. Ni lazima kuwawekea fito kwa kuwa ndege hupenda kupumzika juu ya fito. Ni lazima banda la kuku lifungwe vizuri nyakati za usiku ili kuzuia wanyama wanaoweza kuwadhuru kuku. Ni lazima liwe safi wakati wote ili kuzuia magonjwa kama vile mdondo na mengineyo. Usitumie pumba za mbao au nguo kuukuu kwenye viota vya kutagia kwani huchochea kuwepo utitiri na funza wa kuku. Inashauriwa kutumia mchanga laini.


Maji ya kunywa: Kuku wapatiwe maji safi. Ni lazima kuangalia mara kwa mara na kuyabadilisha maji. Kamwe usiwape kuku maji machafu.


Chanjo: Chanjo kwa mifugo ni lazima ili kuzuia mashambulizi ya magonjwa. Magonjwa yaliyozoeleka ni kama vile Mdondo, Kideri, Ndui ya kuku, na homa ya matumbo (typhoid). Chanjo kwa kawaida hutolewa mara moja kwa kila baada ya miezi miwili.


Uwekaji wa kumbukumbu: Kumbukumbu zijumuishe aina ya ulishaji, namba ya uzalishaji, muda wa mwisho wa matumizi, kiasi cha malisho kwa kila siku, idadi ya vifo, na idadi ya mayai yaliyozalishwa.


Mwanzoni unahitaji nini?


Wafugaji walio wengi wanauliza wanahitaji nini katika hatua za awali ili kuweza kuanzisha mradi wa ufugaji wa kuku. Hii itategemea aina ya kuku uliochagua kufuga.


Ni busara kuwa na vifaa muhimu vinavyohitajika na viwe katika hali ya usafi kabla ya kuweka kuku bandani mwako. Kama unaanza na vifaranga, vifuatavyo ni vifaa muhimu vinavyohitajika kwa ajili ya vifaranga 200.


• Tenga na utengeneze banda zuri lenye joto na hewa ya kutosha wakati wote.

• Vyombo vinne (4) vya kunyweshea maji, hii ni katika wiki 2 za mwanzo na uongeze vyombo taratibu kulingana na kuku wanavyokua.

• Vyombo vinne (4) vya kulishia chakula, na viongezeke kulingana na kuku wanavyokua.

• Matandazo makavu na safi, inaweza kuwa maranda au mabua ya ngano.

• Pakiti moja au mbili za dawa ya Coccid (hii inapatikana katika maduka yote ya kilimo). Hata hivyo, utaratibu wa chanjo ni lazima ukamilishwe.

• Chakula kwa ajili ya vifaranga ambacho kimezalishwa na watengenezaji wanaoaminika.


Ufugaji wa kuku unaweza kuongeza kipato cha familia


“Mimi ni mfugaji mdogo wa kuku wa kienyeji katika viunga vya jiji la Dar es Salaam. Nina kuku 65 ambao ninawafuga katika eneo dogo nyumbani. Nilivutiwa kuanza ufugaji wa kuku wa kienyeji baada ya kutumia fedha nyingi kununua mayai ya kuku wa kienyeji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.


Nilikua natumia zaidi ya shilingi elfu thelathini (30000) kila mwezi kwa ajili ya kununua mayai ya kuku. Ndivyo anavyoanza kusimulia mafanikio yake Bi. Haika Mcharo, ambae ni mfugaji.


Msukumo huu ndio ulinifanya niwe na wazo la kufuga kuku wa kienyeji. Nilianza na kuku 12 na sasa ninao kuku 65 wanaotaga na wanaotarajia kutaga. Sipati faida kubwa sana ila kwa sasa sinunui tena mayai bali ninauza mayai. Faida nyingine ni upatikanaji wa mbolea unaotokana na kinyesi cha kuku. Ninatumia kwa kulimia bustani ya maua na mboga mboga, pia majirani wenye uhitaji wanakuja kwangu kubeba. Kwangu, kufuga kuku wa kienyeji kuna umuhimu sana kwani najiongezea kipato, ni kama akiba ambapo faida yake huzaana tu kama riba ya benki.


Malengo yangu ni kuwa na kuku wengi ambao watagharamia karo ya watoto wangu, malipo ya hospitali na gharama nyingine za nyumbani. Sihangaiki sana katika kupata chakula cha kuku ninaowafuga kwani mbali na mchanganyiko wa chakula ninaowanunulia kwa jina maarufu layers mash pia huwapa mabaki ya chakula, majani, mabaki kutoka jikoni na, vyakula vya kujitafutia muda wa jioni napowafungulia. Mfumo huu wa kufuga kuku kwa njia ya kienyeji unatumia viungo vinavyopatikana kwa urahisi. Huwa ninazingatia tiba mara ninapoona kuku wangu wanadhoofika. Nina daktari maalumu wa mifugo ambaye hunipa ushauri wa tiba ipi niitumie na kwa wakati gani. Pia ninazingatia chanjo zote ili kuwalinda na magonjwa.


Hakuna changamoto kubwa ninayokumbana nayo bali hali ya kuwatunza na kuwalisha inahitaji umakini mkubwa ili wakue na kupata kile ninachokitarajia. Ufugaji wa kuku wa kienyeji ni rahisi na hauhitaji gharama kubwa kwani waweza ukafuga kama kikundi au mtu mmoja mmoja. Nimefanikiwa kuwashawishi akina mama 5 ambao kwa sasa wameanza ufugaji wa kuku wa kienyeji. Lengo ni kuwa na kikundi ambacho tunaweza kupata soko la kuuza mayai kwa uhakika na upatikanaji wake uwe wa uhakika.Mpendwa Mfugaji: Tunatafuta mfugaji ambaye amefanya ufugaji wa kuku wa kienyeji na kupata mafanikio. Tungependa kukupa nafasi ya kushirikisha wafugaji wengine uzoefu wako kupitia jarida hili. Wasiliana nasi kwa kututumia ujumbe mfupi au utupigie simu kupitia namba hizi 0717 266 007, 0785 133 005.

Utunzaji wa udongo kwa ajili ya kilimo hai
January 22nd, 2013
<< rudi


Uelewa wa maisha ya mimea husaidia kwa kiasi kikubwa kwa hatua ya kuchukua kuilisha mimea hiyo.


Utunzaji wa udongo unategemeana kwa kiasi kikubwa na mazingira ya kibiolojia. Kazi kubwa ya baadhi ya viumbe hai waliomo kwenye udongo, ni kumeng’enya mabaki ya mimea na viumbe hai wengine. Mtiririko huu hufanya uwepo wa nguvu, virutubisho, na hewa ya kaboni, ambavyo kwa pamoja hutengeneza rutuba kwenye udongo.


Utunzaji wa rutuba ya udongo unaongozwa na filosofia hii ‘Lisha udongo ili nao ulishe mimea.’ Udongo wenye rutuba utazalisha mimea yenye afya inayoweza kukabiliana na magonjwa. Uzalishaji wa mazao kwa njia za asili uhakikisha kunakuwepo uzalishaji wa kutosha bila ya kutumia pembejeo za ziada isipokuwa matandazo, mboji na bila kutifua udongo mara kwa mara. Ongezeko la malighafi za asili husaidia kuimarisha udongo na kufanya kuwepo kwa virutubisho vya kutosha.


Athari kwa afya ya mimea


Kwa bahati mbaya, aina ya kilimo cha kisasa na kinachotumia kemikali hufanywa tofauti na ilivyo kwa kilimo hai. Katika aina hii ya kilimo; udongo hulimwa mara kwa mara jambo linalosababisha uharibifu wa muundo wa udongo, uwiano wa virutubisho, ambapo virutubisho huongezwa kwa kutumia mbolea za viwandani na matandazo hayazingatiwi. Muundo wa udongo unapobadilika, rutuba nayo hupungua, uwezo wa udongo kwenye udongo pia hupungua.


Kiwango cha udongo mzuri pia hupungua kwa kuwa hakuna tena viumbe hai wanaotengeneza udongo ila unapungua kila msimu wa mavuno. Kwa asili mzunguko huu huwa na matokeo yanayoishia kwenye afya ya mimea, na hapa wadudu huchukua nafasi inayowawezesha kufikia malengo yao.


Ziba pengo


Wakulima wanatakiwa kuhakikisha kuwa kuna virutubisho vya kutosha shambani mwao kila wakati. Ikiwa kuna mwanya pale ambapo baadhi ya pembejeo zinakosekana, kununua virutubisho kwa ajili ya udongo vilivyomo kwenye mfumo wa mbolea za asili inaruhusiwa. Hata hivyo, weka utaratibu wa kuwa na virutubisho kutoka shambani mwako muda wote.


Endapo tukitegemea kulisha udongo kutokana na mbolea za viwandani na kutumia virutubisho vya asili, bado tutakuwa tunafanya sawa na yanayofanyika katika kilimo cha kisasa. Tutakuwa hatujauongezea udongo uwezo wa kujitengeneza na kuongezeka, jambo ambalo ndio msingi muhimu wa kilimo hai.


Vyanzo vya virutubisho


Mimea inayofunika udongo – Mimea inayotambaa huongeza na kushika virutubisho kwenye udongo, kuongeza malighafi zinazooza kwenye udongo, kuzuia madini ya naitraiti kuzama kwenye udongo, virutubisho kutiririshwa, na mmomonyoko wa udongo. Jambo la muhimu hapa ni kuwa udongo umefunikwa ili kuzuia uharibifu. Mimea jamii ya mikunde inapendekezwa zaidi kwa kuwa

husaidia kuongeza nitrojeni kwenye udongo inayopatikana hewani.


Inashauriwa pia kuchanganya mimea jamii ya mikunde na nyasi kwa kuwa nyasi hutumia nitrojeni nyingi sana kutoka kwenye udongo, hivyo itasaidia kutokuharibika kwa mtiririko mzima wa uwekaji wa nitrojeni kwenye udongo.


Mboji - Mboji hasa inayotengenezwa kwa kutumia kinyesi cha wanyama, inaweza kuwa chanzo kizuri cha viumbe wadogo kwenye udongo na virutubisho vyenye gharama ndogo. Unapotumia mboji, changamoto kubwa ni kuhakikisha kuwa imeoza vizuri na namna ya kuitumia kwa usahihi. Endapo mchanganyiko uliotumika kutengeneza mboji hiyo yalikuwa na ubora wa chini, basi mboji hiyo nayo itakuwa na ubora mdogo sana. Itakuwa vizuri kama wakulima hawataacha mboji ikapigwa na jua au mvua, kwa kuwa hali hii inaweza kusababisha kupotea kwa virutubisho kwenye mboji. Kinyesi cha mifugo huboresha mboji zaidi.


Utafiti wa hivi karibuni unaonesha kuwa kiasi cha 15% ya virutubisho vinavyopatikana kwenye mboji hutumika shambani kwa mwaka wa kwanza. Hivyo, matumizi ya mara kwa mara ya mboji yanapendekezwa ili kuweza kuongeza nitrojeni na malighafi zinazo oza kwenye udongo.


Samadi - Samadi inayotokana na wanyama waliokomaa inaweza kuwa na uwiano mzuri wa virutubisho vya nitrojeni na aina nyingine kwa kiasi kidogo. Tatizo moja la samadi ni upatikanaji pamoja na kutokuwa na ubora unaofanana wakati wote. Kiasi kikubwa cha samadi inayotumika kwenye shamba la mboga, huozeshwa kabla ya kutumika, jambo linalosaidia kupunguza madhara kwenye vyakula.


Malengo kwa ajili ya udongo na mazao

•  Kuongeza malighafi zinazo oza kwenye udongo

• Kuboresha muundo wa udongo

• Kuwezesha upatikanaji wa nitrojeni

• Kuongeza uwezo wa uhifadhi wa rutuba

• Kujenga uwepo wa uhai wa viumbe hai kwenye udongo

• Kufifisha magonjwa ya mazao

• Kujenga mazingira ya udongo wenye uwiano


Pandikiza parachichi upate mavuno zaidi
January 22nd, 2013
<< rudi


Msukumo wa uhitaji mkubwa wa parachichi kwa wingi na zenye ubora unawasukuma wakulima kutumia teknolojia mpya.


Upandikizaji hujumuisha aina mbili za mimea. Unachukua mmea mmoja ambao unadhani hauna tija nzuri, na sehemu ya mmea mwingine ambao una ubora zaidi na kupandikiza kwa kukata na kufunga pamoja ili kupata mbegu bora zaidi. Utaratibu wa kupandikiza hivi sasa umekuwa silaha ya wakulima kuwakomboa dhidi ya wadudu pamoja na magonjwa, na hili kwa sasa halifanyiki tena maabara kama ilivyokuwa awali na hii inadhibitishwa na yale tuliyojionea Njombe tulipotembelea wakulima.


Kwenye shamba la bwana Bosco Kidenya, ana kitalu chenye zaidi ya miche 1200 ya miparachichi, baadhi ikiwa tayari imeshapandikizwa na mingine ikiwa inasubiri kufikia wakati wa kupandikiza.  Huyu ni mmoja kati ya wakulima walio wengi wanaofanya kazi kwa karibu na CARITAS Njombe, kuboresha uzalishaji wa parachichi, pamoja na kuboresha kipato cha wakulima ambao wanazalisha matunda na mboga mboga.


Mbinu wanayotumia


Wakulima hukusanya kokwa za parachichi kutoka maeneo ya sokoni; wanachofanya ni kuhakikisha tu kuwa mbegu hiyo ni safi, haijaathiriwa na magonjwa na itaota. Baada ya hapo huchagua zile zenye muundo mzuri na kuzipanda kwenye boksi au kwenye sehemu ya kitalu. Baada ya kuota huziotesha kwenye makopo, au kwenye viriba kisha kuendelea kumwagilia maji mpaka zinapokuwa na umbo usawa wa penseli. Upandikizaji ni lazima ufanyike wakati mmea umefikisha unene wa penseli. Kupandikiza kwa kutumia chipukizi lililolingana na mche unaopandikizia ni njia yenye mafanikio zaidi.


Upandikizaji ni lazima ufanyike wakati ambao mizizi bado ni laini. Pandikizi litakalotumika wakati wa kupandikiza ni lazima lisiwe katika hatua ya ukuaji kwa wakati huo, na ni lazima umbo liwiane na mti linapopandikizwa kuzuia maji yasipotee na kusababisha pandikizi kukauka.


Mapandikizi ni lazima yatokane na aina ya parachichi ambazo zimeboreshwa kama vile hass, fuerte  au puebla. Kwa wale wakulima ambao mmea utatoa majani mapya. wana mkataba na Africado, watahitajikupata mapandikizi kutoka kwenye miti ya hass. Hii ina maanisha kuwa mkulima anayetaka kuanzisha kitalu kwa ajili ya kupandikiza ni lazima apande walau miti 5 ya parachichi aina ya hass ili kupata mapandikizi.


Njia ya kupandikiza ina ufanisi zaidi na ni rahisi kuliko kupanda miche upya, kwa kupandikiza inagharimu chini ya asilimia 75, kuliko kupanda miche upya na kuweza kupata aina ambayo inastahimili magonjwa. Wakulima pia wamekuwa na rikodi nzuri ya ongezeko la mavuno kutokana na mimea waliyopandikiza, pamoja na upungufu wa matumizi ya madawa.


Wakulima ambao wanafanya kazi zao chini ya CARITAS Njombe sasa wanaona faida kubwa inayotokana na kupandikiza, wameamua kuwekeza kwenye utaalamu huu na kuwa na miche mingi kwenye vitalu vyao. Hii ni mbinu ya kilimo ambayo ina faida kubwa kwa mkulima, huku akiwa amewekeza kwa kiasi kidogo sana katika kukabiliana na wadudu na magonjwa na kuepuka kuwa na mazao yenye ubora wa chini.


Namna ya kupanda


Nafasi halisi inayohitajika na mmea wa parachichi ili ukae vizuri ni nafasi ya 9m x 9m. Chimba shimo katika vipimo vya 60sm x 60sm kwa 60sm kwenda chini kisha tenga udongo wa juu na wa chini. Changanya udongo wa juu na mbolea ndoo moja iliyooza vizuri, pamoja na kiganja kilichojaa cha mbolea ya minjingu.


Ondoa mche wako kwenye kiriba ulipopandwa. Hii itakuwa rahisi zaidi endapo ulikuwa umenyweshea muda kidogo uliopita. Panda kwa kutumia udongo wa juu uliochanganya na mbolea na uweke mpaka kujaza shimo.


Mwagilia maji mara baada ya kupanda. Funika mmea mchanga kwa kutumia majani ya migomba au aina nyingine ya majani yanayofanana na hayo, mpaka kufikia kipindi ambacho mmea utatoa majani mapya.


Taarifa hii imeandaliwa kutokana na tuliyojionea tulipomtembelea shamba la bwana Bosco Kidenya kutoka Njombe, ambaye ni msomaji mzuri wa jarida la Mkulima Mbunifu. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu +255 753431117.


Hifadhi mayai wa kwa muda mrefu
January 22nd, 2013
<< rudi


Wakulima wanaowekeza kwenye mradi wa kuku, hupata hasara pale ambapo hawatunzi mayai ipasavyo.


Mayai ni bidhaa hafifu na inayoharibika kwa haraka. Hivyo, ni lazima ishikwe kwa uangalifu na kutunzwa vizuri baada ya kutagwa ili yasivunjike au kuharibika. Watu wengi wanaonunua mayai kutoka dukani watatambua mara moja kuwa mayai hayo yamevunjika au yameoza. Tatizo hili linaweza kutokana na utunzaji na uhifadhi wakati mayai bado yakiwa kwa mfugaji.


Ili kupunguza hasara, ni lazima mfugaji ahakikishe kuwa mayai yanafika sokoni yakiwa bado mapya na salama. Utunzaji sahihi wa mayai huyafanya yaepukane na madhara yanayoweza kutokana na viumbe wadogo wadogo kama vile bakteria, wanyama walao mayai, upotevu wa unyevu, au joto wakati wa uhifadhi na kusafirisha kwenda sokoni, jambo linaloweza kuyafanya yavunjike. Mayai kama ilivyo kwa viumbe hai wengine yanahitaji kupumua. Trei za kuhifadhia mayai ziwekwe kwenye sehemu yenye hewa inayozunguka, hasa hewa ya oxyjeni.


Trei zote za kuhifadhia mayai ni lazima ziwekwe katika hali ya usafi, zisiwe na harufu ili kuepuka kufishwa au kusababisha hali yoyote inayoweza kusababisha uharibifu. Mayai ni lazima pia yakingwe dhidi ya joto kali pamoja na unyevu.


Weka sehemu yenye ubaridi


Mayai yanaweza kuharibika kwa haraka kutokana na joto kali. Labda yahifadhiwe kwenye jotoridi la chini, vinginevyo mfugaji atapoteza idadi kubwa ya mayai kabla hayajafika sokoni. Ni lazima kuhakikisha kuwa mayai yanahifadhiwa sehemu yenye ubaridi, ambayo siyo kavu sana, vinginevyo yatapoteza unyevu kwa haraka endapo yatawekwa sehemu kavu. Hali ya mahali pa kuhifadhia inategemea na siku ambazo mfugaji anahitaji kuhifadhi mayai.


Wafugaji wenye uzoefu wamekuwa na uwezo wa kuhifadhi mayai kwa kipindi cha miezi 6-7 kwa kutumia jokofu. Wafugaji wadogo pia wanaweza kuhifadhi mayai kwa siku kadhaa mpaka watakapopata mayai kwa ajili ya kuhatamiwa. Kamwe usihifadhi mayai unayokusudia kutumia kwa ajili ya kuhatamiwa kwenye jokofu.


Uhifadhi wa mayai kwa ajili ya kuhatamia


Wafugaji wadogo hutumia njia ya kiasili kuhatamisha na kuangua mayai. Hii ni njia ya kutumia kuku au ndege mwingine ambaye hupewa mayai na kuyahatamia hadi kuanguliwa. Kuku wa kienyeji ni wazuri sana wanapotumiwa kwa ajili ya uzalishaji wa vifaranga. Hata hivyo kwa uzalishaji mzuri ni lazima mfugaji ahakikishe kuwa kuku anapewa mayai yenye uwezekano mkubwa wa kuanguliwa.


Mbinu moja wapo ambayo mfugaji anaweza kuitumia kutambua mayai yenye uwezekano mkubwa wa kuanguliwa ni kwa kumulika kwa kutumia mshumaa. Mayai yanaweza kuwekwa kwenye mwanga mkali ambao utakuwezesha kuona ndani ya yai. Kifaa rahisi cha kumulika mayai kinaweza kutengenezwa kutokana na kuweka balbu ndani ya boksi dogo. Unakata tundu dogo kuruhusu mwanga. Hakikisha linakuwa na ukubwa wa kuweza kuruhusu yai kukaa juu yake.


Shika yai kwa kulisimamisha kwa kutumia vidole vyako viwili, kasha liweke kwenye mwanga wa tochi au balbu. Zoezi hili linakupa uhakika kuwa mayai yenye uwezekano wa kuanguliwa ndiyo pekee yanayochaguliwa.


Tengeneza sehemu ya kuhatamia mayai


Mfugaji anaweza kuboresha uzalishaji wa kuku wa kienyeji kwa kuwajengea tabia ya kuhatamia mayai. Kuku wa kienyeji wakiwa wamelishwa vizuri, wanaweza kuhatamia kati ya mayai 10-14 kwenye mzunguko mmoja. Baada ya kuangua, mfugaji amruhusu kuku kukaa na vifaranga walau kwa wiki moja. Baada ya hapo vifaranga wanaweza kutengwa.


Kuku wakiwa bado katika hali ya kuhatamia, anaweza kupewa mayai ya bandia ambayo yanaweza kutengenezwa kutokana na sabuni, huku kuku wengine wakiwa wamehatamia mayai halisi ya kutosha. Mayai bandia yanaweza kuondolewa na kuku kuwekewa mayai halisi aendelee kuhatamia mpaka yatakapoanguliwa.


Kuku wanaohatamia ni lazima wapatiwe chakula na maji ya kutosha. Kuku ambao hawahitajiki kwa ajili ya kuendelea kutotoa, wanyang’anywe vifaranga na kuachiliwa walipo kuku wengine. Ni vizuri kuweka alama kila yai kuonesha ni tarehe gani lilitagwa, hii itamsaidia mfugaji kutokuchanganya mayai ya zamani na mayai mapya. Badala yake, mfugaji anaweza kuwatenga kuku ambao amewaandaa

kwa ajili ya kutotoa na wale ambao ni kwa ajili ya kutaga tu ili asichanganye mayai yake.


Jinsi ya kutunza vifaranga


• Vifaranga wanapotengwa na mama yao, wawekwe pahali safi.

• Ni lazima wapatiwe joto kutoka kwenye taa ya kandiri.

• Vifaranga walishwe kwa kutumia chakula maalumu kwa ajili ya vifaranga, kasha waongezewe glukosi na maji safi. Hii itawawezesha kukua kwa haraka.

• Sehemu wanapokuziwa vifaranga ni lazima kupima joto mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa hawapati joto la kuwazidi au kwa kiwango cha chini.


Guatemala: Malisho wakati wa kiangazi
January 22nd, 2013
<< rudi


Majani haya yanatumika kama chakula cha ziada kwa mifugo wakati wa kiangazi, hayatakiwi kutumika kama malisho pekee.


Majani aina ya Guatemala (Tripsacum andersonii) imesambaa kwa kiasi kikubwa katika ukanda wa tropiki. Aina hii ya majani inahitaji kiasi kikubwa cha mvua, au udongo wenye unyevu, lakini hata hivyo huweza kubaki yakiwa na kijani kibichi wakati wote wa kipindi cha kiangazi.


Nchini Tanzania, majani haya yanapatikana kwenye nyanda za kati, na sehemu zenye miinuko, hasa zenye rutuba ya kutosha kama vile kwenye safu za mlima Kilimanjaro, mlima Meru na Milima ya Usambara. Mimea hii inakuwa kwa wingi, na inafaa zaidi kama chakula mbadala kinachotumika kwa ajili ya mifugo wakati wa kiangazi. Guatemala ina uvumilivu zaidi ya matete (napier grass), lakini ni dhaifu katika uzalishaji na ina virutubisho vichache sana.


Kupanda


Guatemala hupandwa kutokana na vipande vya mashina, na huwa tayari kuvunwa baada ya miezi. Hakikisha kuwa unapata mapandikizi kutoka kwenye chanzo kinachoaminika. Unaweza kupanda kipande cha shina chenye pingili 3, au sehemu ya shina iliyoanza kuota kwa kulaza chini, kwenye sehemu yenye nafasi ya ½ mita x 1 mita. Inahitaji mbolea nyingi kwa ajili ya ukuaji mzuri.


Mseto


Guatemala inaweza kupandwa mseto na desmodium, leucaena, sesbania, au calliandra ili kuongeza mavuno ya malisho makavu yenye protini kwa wingi.


Mavuno na matumizi


Hekari moja ina uwezo wa kuzalisha Guatemala kiasi cha tani 9-22, yakiwa yamekatwa kiasi cha sentimita 10-25 kutoka kwenye usawa wa ardhi. Guatemala hasa hutumika kama akiba ya malisho ambayo hukatwa na kulishwa mifugo wakati wa kiangazi yakiwa mabichi. Majani haya hutengeneza sileji yenye ubora wa wastani. Majani haya yanaweza pia kutumika kama uzio sehemu ya kuishi, au kwenye kontua kwa ajili ya kuzuia mmomonyoko wa ardhi, matandazo shambani, au kwa ajili ya kukausha maji sehemu yenye tindiga. Inatumika pia kama kizuizi cha baadhi ya wadudu kwenye chai, kahawa na viazi.


Guatemala haiwezi kuvumilia kuchungia mifugo au kukatwa mara kwa mara. Haishauriwi kuchungia mifugo kwenye aina hii ya malisho. Inashauriwa kukata kwa uwiano wa siku 30 wakati wa mvua, na uwiano wa siku 42-45 wakati wa kiangazi. Ilikuepuka kuvimbiwa, inashauriwa kukata na kuacha majani haya yanyauke kabla ya kulishia mifugo.


Ubora wa virutubisho


Kwa kiasi kikubwa hii inategemeana na ukataji wa mara kwa mara, mashina yakikomaa yanakuwa na nyuzi nyingi na pia kuwa na kiasi kidogo cha protini na wanga kama hayakutunzwa na kuwekwa mbolea vizuri. Wakati wa hatua tofauti za matumizi, kiasi cha protini pia hutofautiana. Sehemu ya juu iliyokauka inakuwa na asilimia 6.4, sehemu ya juu ambayo ni mbichi inakuwa na asilimia 8.8, sehemu ya majani ambayo ni mabichi inakuwa na asilimia 6.1, shina linakuwa na asilimia 4.6. Kiwango cha protini kinakuwa juu wakati wa wiki 3, na kuzidi kupungua kadri yanavyozidi kukomaa na nyuzi nyuzi kuongezeka.


Majani yanakuwa na kiasi kikubwa cha madini aina ya manganese, chuma, zink na potashiamu. Kutokana na kiasi kidogo cha protini kwenye aina hii ya malisho, malisho mbadala yenye kiasi kikubwa cha wanga na protini inafaa kutumika kwa pamoja na Guatemala kwa ukuaji mzuri wa mifugo. Miongoni mwa vyanzo vya protini vilivyothibitishwa ni pamoja na vyakula vyenye mchanganyiko wa samaki, soya, aina hii ya malisho huwa na matokeo mazuri zaidi kuliko vyakula vinavyotokana na mashudu ya pamba, hasa kinapotolewa kwa kiwango cha kutosha pamoja na majani ya Guatemala.


Miti ya malisho


Guatemala inaweza kupandwa mseto na miti ya malisho. Kwa kufanya hivyo, mkulima anaweza kupunguza au kuondokana kabisa na matumizi ya virutubisho. Utafiti unaonesha kuwa kilo 3 za malisho yanayotokana na miti kama vile calliandra, leucaena, desmodium , viazi vitamu, haradali na aina nyingine za jamii ya mikunde zina virutubisho sawa na pumba aina ya diary meal. Mfugaji anaweza kupunguza gharama kwa kutumia aina hii ya malisho kwa ajili ya mifugo wake.


Ni muhimu kwa mkulima kufahamu kuwa ng’ombe wa maziwa wanahitaji mlo kamili wenye kutia nguvu, protini na vitamini. Mlo huo ni lazima uwe na wanga kiasi cha asilimia 75, Protini asilimia 24 na asilimia 1 ya madini.


Taarifa hii imeandaliwa kujibu swali lililoulizwa na kikundi cha wakulima cha MOWE kutoka Machame Mkoani Kilimanjaro.


Jumuisha miti kwenye shamba
January 22nd, 2013
<< rudi


Upandaji wa miti unalenga kupunguza madhara yanayotokana na uharibifu wa misitu, pamoja na kutumia ardhi kupita kiasi.


Uoto wa asili kama hautaingiliwa na shughuli za kibinadamu, ni mwanzo mzuri wa uwiano wa maji. Miti na vichaka ni kiashirio kizuri cha maji katika ukanda wowote. Katika ukanda wa tropiki wenye mvua nyingi, misitu yenye mvua nyingi na virutubisho vinavyotokana na mimea na wanyama vina nguvu zaidi. Kwenye ukanda wenye mvua kidogo, miti hupukutisha majani wakati wa kiangazi, hivyo kufanya uzalishaji wa mimea kuwa hafifu. Sehemu yenye mvua hafifu miti hunyauka, wakati ukanda wa savanna na miti hutawala zaidi.


Miti ni sehemu muhimu ya uwiano wa maji


Inahifadhi maji kwenye ukanda wa mizizi, kukinga udongo usikauke, kujenga tabaka la udongo, na kusaidia kuhifadhi maji. Matandazo yanayotokana na majani ya miti hukusanya matone ya mvua na kuhifadhi kwa muda, kuzuia mmomonyoko wa udongo, pia kuchuja maji yanayoingia ardhini taratibu. Miti hurudisha maji kwenye mzunguko kwa njia ya mvuke, na kuchangia katika kuunda mawingu ya mvua.


Endapo miti ikiondolewa, maji yote yataondoka na kupotelea ardhini kisha kuondoka kabisa kwenye mzunguko, huku yakichukua virutubisho na tabaka jembamba la udongo. Utafiti wa misitu na mbinu ya kujumuisha miti na vichaka kwenye mashamba ya kilimo, imekuwa mbinu muhimu ya kuzuia uharibifu wa udongo.


Weka nafasi nzuri ya miti kwenye shamba lako.


Miti kwenye shamba la mazao husaidia kurekebisha hali ya hewa, kuzuia maji kutiririka kwa kasi, kuhifadhi udongo na maji, kutoa malighafi zinazo oza kwa ajili ya udongo, na kuweka kivuli kwa ajili ya mimea. Pia ni chanzo cha chakula, malisho, nishati, na nguzo. Kutegemeana na aina ya miti na mazao yaliyopandwa, kwa kawaida hupandwa kwa nafasi ya mita 8 mpaka 10 au zaidi, ili kupunguza ushindani. Mizizi mirefu, na miti inayoongeza  nitrojeni kwenye ardhi inapendekezwa zaidi.


Mbali na Lusina leucocephala, ambazo hazistawi vizuri katika ukanda wenye ukame, Sesbania sesban, Crotalaria grahamiana, Tephrosia vogelii,  na Gliricidia sepium inapendekezwa, lakini miti ya matunda au yenye kokwa inafaida zaidi.


Mfano mzuri ni:

•  Miti ya matunda katika bustani ya nyumbani.

•  Miti ya kivuli katika shamba la kahawa, ina faida zaidi. Inazuia madhara yanayoweza kusababisha kutokuchanua kwa mimea katika majira ya mwaka. Hii inaweza kuongeza maisha ya mibuni mara mbili zaidi! Kwenye sehemu za miinuko, inasaidia kudhibiti mmomonyoko wa ardhi pia.

• Grevillea robusta  ni miti mizuri sana ya kivuli shambani mwako.


Tawanya miti kwenye shamba lako


Kwenye njia hii ya asili, miti huhifadhiwa kwa ajili ya mifugo kujitafutia malisho, kivuli, na mara nyingine kwa ajili ya matumizi mengine. Miti jamii ya mikunde ambayo ina kiasi kikubwa cha protini hufanya mifugo kufidia virutubisho wanavyokosa wakati wa kiangazi, na kusaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa.


Uchochoro wa mazao


Kulima kwa uchochoro au mseto wa miti hufanyika pamoja na zao la msimu. Mbinu hii inafaa zaidi kwenye udongo wenye unyevu mwingi, lakini ukiwa na tatizo la rutuba. Miti ya Sesbania sesban inapopandwa kwenye  shamba la nafaka husaidia kuongeza uzalishaji wa mahindi. Miti ni lazima itunzwe vizuri na kukatiwa mara kwa mara. Matawi yanayokatwa hutumika kulisha mifugo, kama matandazo kwenye shamba la mahindi kuboresha rutuba kwenye udongo, kufifisha magugu, na kwa ajili ya kuni, au nguzo. Kwa bahati mbaya, kuna ushindani mkubwa baina ya aina ya miti ya mbao na mazao kwenye eneo kame.


Uzio


Mstari wa miti au vichaka vinavyopandwa kando kando ya mipaka ya shamba. Hata hivyo huu ni utamaduni wa zamani sana, aina mbalimbali za mimea zinaweza kutumika. Endapo itapandwa kwa kusongamana, inaweza kusaidia kuzuia wanyama kuingia kwenye mazao. Fito au matawi yaliyokufa inaweza kusimikwa katikati yake, au waya unaweza kutumika kuweka uzio. Inatoa kuni kwa matumizi ya nyumbani, malisho, na kivuli kwa ajili ya mazao na wanyama, kuzuia upepo, matawi yaliyokatwa yanaweza kutumika kutengeneza uzio pia.


Akiba ya malisho


Majani ya miti husaidia wakati kuna uhaba wa malisho hasa wakati wa kiangazi. Ulishaji wa virutubisho mbadala vinavyotokana na Calliandra, Leucaena diversifolia, Gliricidia sepium, na vinginevyo huongeza uzalishaji na ubora wa maziwa kwa wanyama wa maziwa, na pia hupunguza gharama ya chakula kwa ajili ya ng’ombe wa maziwa. Lisha kiasi cha asilimia 30 ya majani kutoka kwenye miti ya malisho.


Karoti inahitaji palizi ya mara kwa mara
September 12th, 2012
<< rudi


Nimepanda karoti lakini sitaki kutumia dawa za viwandani kuua magugu mbali na kupalilia kwa mikono ni dawa gani za asili ninazoweza kutumia kuua magugu?


Magugu ni tatizo kubwa kwa karoti.  Hii ni kwa sababu ni zao linalokuwa taratibu na pia majani yake si mapana kuweza kuweka kivuli halikadhalika kupambana na wadudu. Magugu yasipodhibitiwa, yataathiri mavuno kwa kiasi kikubwa. Kwa bahati mbaya hakuna dawa za asili za kuulia magugu. Viini vyovyote vinavyoweza kutumika kuulia magugu ni wazi kuwa pia vinaweza kuathiri mazao pia. Hivyo, wakulima wanaofanya kilimo hai hufanya palizi kwa kutumia mikono au mashine.

Utunzaji wa karoti kwa njia ya kilimo hai, ni lazima uanze hata kabla ya wakati wa palizi. Panda karoti sehemu ambayo haina magugu mengi, na ambayo haija athiriwa sana na magugu kama vile mbaruku, mtunguja na nyasi.  Panda karoti kwenye sehemu uliyovuna mazao kama vile maboga, matango, tikiti, vitunguu au spinachi.  Baada ya kuvuna mazao yaliyotangulia, lima shamba lako na upande mbegu za karoti kwenye kitalu kisichokuwa na magugu.

Udongo ni lazima uvunjwe vizuri ili kuepusha hali itakayozuia mizizi kwenda chini ipasavyo. Karoti inahitaji udongo unaoweza kuruhusu kwenda chini vizuri, na unaopitisha maji vizuri, na wenye kiasi kikubwa cha malighafi zinazo oza (udongo mweusi). Utunzaji wa udongo kwa ajili ya kilimo hai, ni pamoja na kuweka mbolea vunde, pamoja na matandazo ambayo huongeza rutuba kwenye udongo kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo wakati wa kupanda karoti, inabidi shamba lisiwe na mabaki ya mazao ambayo hayaozi kwa kuwa yanaweza kuathiri uotaji wa mbegu za karoti. Endapo dawa za kuulia magugu zitatumika, inabidi zitumike kabla ya kupanda kwa kuwa zinaweza kuuwa miche ya karoti pia.

Karoti zinahitaji kukua kwa haraka bila vipingamizi ili kuwa na majani pamoja na mizizi iliyo imara. Kupalilia mapema ni muhimu ili kuepuka upotevu wa mavuno, hasa katika wiki 10 za mwanzo toka kuota. Wakulima wa karoti hutumia jembe la mkono kupalilia kati ya mstari na mstari wa miche ya karoti. Lakini magugu yanayo ota katikati ya karoti ni lazima yang’olewe kwa mikono. Kuwa makini ili usijeruhi mimea! Kwa kawaida kupalilia kwa kutumia jembe la mkono hufanyika mara 3 katika kipindi chote cha ukuaji.


Vitunguu, kiungo cha chakula chenye faida kwa mkulima
September 12th, 2012
<< rudi


Hapo awali kitungu kilikuwa ni zao lililokuwa linapatikana porini katika ukanda wa bahari ya Mediterania. Zao hili hulimwa katika nchi nyingi za magharibi, nchi za milima zilipo kaskazini mwa dunia, likwemo bara la Afrika. Vitunguu hustawi katika hali ya hewa ya jotoridi 13°C – 24°C, hali ya hewa inayofaa kwa kuotesha na kukuzia miche kwenye kitalu ni jotoridi 20°C – 25°C. Kwa kawaida vitunguu huhitaji kiasi cha joto nyuzi 20°C-25°C ili kuweza kustawi na kukua vizuri. Joto zaidi ya hapo hufanya vitunguu kudumaa na kutoweza kutengeneza viazi (bulbs).

Matumizi

Kitunguu hutumika kama kiungo cha kuongeza ladha kwenye chakula, na pia hutumika kama dawa ya kansa ya tumbo, vidonda na majipu.

Ustawi

Zao la vitunguu hustawi katika udongo wa tifu tifu wenye mbolea ya kutosha, ukiwa na uchachu wa udongo (PH) kiasi cha 6 – 6.8.  Udongo wa mfinyanzi haufai kwa zao la vitunguu kwa kuwa hauruhusu viazi vya vitunguu (bulbs) kutanuka.  Hivyo uwezekano wa kupata mazao ni mdogo. Pia udongo wa kichanga haufai kwa zao la kitunguu kwa kuwa hauna mbolea na hivyo vitunguu huwa vidogo sana, jambo ambalo ni vigumu kupata mazao yanayofaa kwa soko.

Zao la kitunguu huhitaji unyevu muda wote wa ukuaji wake. Zao hili lina mizizi mifupi hivyo linahitaji kumwagiliwa maji mara kwa mara.

Aina za vitunguu

Kuna aina mbili za vitunguu ambazo zimezoeleka:

• Vitunguu vya asili kama vile Singida, na Rujewa (aina hii ina rangi ya kahawia iliyopauka).

• Chotara: Hii ni aina ya vitunguu inayojulikana kama vitunguu vya kisasa. Katika kundi hili kuna vitunguu kama Texas grano, Red creole, Bombay red, White granex, na Super rex.


Mgawanyiko

Zao la vitunguu limegawanyika katika makundi mawili. Hii inatokana na uhitaji wa mwanga na ukuaji wake.  Aina ya kwanza inahitaji mwanga kwa saa 8-13 ili kuweza kuchanua na kutoa mbegu.

Aina ya pili inahitaji mwanga kwa saa 13-15 kuweza kuchanua na kutoa mbegu.

Kupanda

Vitunguu hupandwa kwa kutumia mbegu ambazo husiwa kwenye vitalu.  Kitalu kinaweza kuwa na upana wa mita 1, urefu unategemeana na ukubwa wa eneo ulilo nalo.

Unaweza kupanda vitunguu kwenye matuta mbonyeo (Sunken bed). Aina hii ya upandaji hutumika kwenye eneo lenye shida ya maji. Upana wa tuta uwe mita moja.

Kupanda kwenye matuta mwinuko (Raised bed) upandaji wa iana hii hutu mika sehemu yenye maji mengi au yanayotuama.

Tahadhari: Maji yakituama kwenye vitunguu hufanya vitunguu kuoza, hivyo kuathiri mavuno.

Nafasi

Vitunguu vipandwe kwa nafasi ya sentimita 7.5 kutoka mche hadi mche, sentimita 12.5 kutoka mstari mmoja hadi mwingine kwenye matuta.

Mbole ya kupandia

Unaweza kutumia mboji, au samadi iliyo oza vizuri kupandia. Baada ya hapo unaweza kuongeza mboji baada ya miezi miwili. Endapo unafanya kilimo kisichozingatia misingi ya kilimo hai, unaweza kupanda kwa kutumia mbolea aina ya NPK (20:10:10) baada ya mwezi na nusu, unaweka mbolea ya Urea.

Palizi

Vitunguu ni zao lenye uwezo mdogo sana wa kushinda na magugu. Hivyo, inabidi shamba liwe safi muda wote wa ukuaji hadi kuvuna.

Uvunaji

Kwa kawaida, vitunguu huchukua muda wa miezi 5-6 tangu kupandwa hadi kuvunwa. Unaweza kuanza kuvuna vitunguu baada ya asilimia 75 ya shingo za vitunguu kuvunjika.  Baada ya kuvuna, unaweza kuweka kwenye madaraja (grades) kwa kufuata ukubwa, rangi na unene wa shingo ya kitunguu. Vitunguu vyenye shingo nyembamba hudumu zaidi, vyenye shingo nene huoza haraka.

Ukataji

Hakikisha kuwa shingo ya kitunguu inabaki kiasi cha sentimita 2. Hii husaidia kuzuia kuoza haraka.

Namna ya kuhifadhi vitunguu

Baada ya kuvuna, hifadhi vitunguu kwenye kichanja chini ya kivuli na uvitandaze vizuri.  Unaweza kuhifadhi vitunguu kwa kufunga kwenye mafungu na kuvitundika.  Vitunguu vikihifadhiwa vizuri vinaweza kukaa hadi miezi minne bila kuharibika, hii hutegemeana na aina ya uhifadhi.

Wadudu wanaoshambulia vitunguu

Kuna aina nyingi za wadudu wanaoweza kushambulia vitunguu.  Hawa wafuatao ni baadhi ya wadudu waliozoeleka kwenye zao la vitunguu.

Thiripi

Thiripi (Thrips): Wadudu hawa hukaa kwenye jani sehemu inayokutana na shina. Wadudu hawa hufyonza maji kwenye majani ya vitunguu na kusababisha majani kuwa na doti nyeupe.

Madhara: Husababisha vitunguu kudumaa hivyo kuathiri ukuaji wake jambo ambalo huathiri mavuno pia.

Kimamba

Kimamba: Wadudu hawa hufyonza maji kwenye vitunguu, na kusambaza ugonjwa wa virusi. Husababisha kudumaa kwa vitunguu. Wadudu hawa ni hatari zaidi kwa kuwa husambaza virusi vinavyoingia hadi kwenye mbegu.

Minyoo fundo (Nematodes): Aina hii ya minyoo hushambulia mizizi ya vitunguu. Hali hii husababisha kudumaa kwa vitunguu kwa kuwa hushindwa kufyonza maji na chakula kutoka ardhini.

Vidomozi (Leaf minor): Hushambulia majani kwa kujipenyeza kwenye ngozi ya jani na kusababisha michoro ambayo huathiri utendaji wa majani.

Utitiri mwekundu (Red spider mites): Wadudu hawa hufyonza maji kwenye majani na kusababisha vitunguu kunyauka.

Funza wakatao miche: Funza hawa hutokana na wadudu wajulikanao kama Nondo, na hushambulia shina na kulikata kabisa.

Namna ya kukabiliana na wadudu hawa

Unaweza kukabiliana na wadudu hawa kwa kufanya kilimo cha mzunguko.  Usioteshe vitunguu sehemu moja kwa muda mrefu, au kufuatanisha mazao jamii ya vitunguu kama vile leaks.

Tumia mbegu bora zilizothibitishwa kutoka kwenye kampuni zinatambuliwa kisheria na kibiashara.  Kupanda kwa wakati unaotakiwa; vitunguu visipandwe wakati wa kiangazi. Vipandwe wakati wa majira ya baridi na kuvunwa wakati wa joto. Tumia dawa za asili za kuulia wadudu, au dawa nyinginezo zinazopendekezwa na wataalamu wa kilimo.

Magonjwa yanayoshambulia vitunguuPurple blotch

1. Purple blotch: Ugonjwa huu husababishwa na ukungu (fungus). Ugonjwa huu husababisha mabaka ya zambarau na meusi katika majani ya vitunguu.  Ugonjwa huu hutokea wakati wa unyevu unyevu mwingi.
Madhara: Ugonjwa huu hupunguza mavuno mpaka asilimia hamsini (50%).

2. Stemphylium leaf blight: Hukausha majani kuanzia kwenye ncha hadio kwenye shina.; Ugonjwa huu hutokea wakati wa unyevu na ukungu mwingi.
Madhara: Hupunguza mavuno hadi kwa asilimia sabini na tano (75%).

Onion yellow draft virus

3. Magonjwa ya virusi (Onion yellow draft virus): Ugonjwa huu husababisha vitunguu kuwa na rangi iliyochanganyika, kijani na michirizi myeupe au njano.  Vitunguu hudumaa kwa kiasi kikubwa;Ugonjwa huu husababishwa na kimamba.
Madhara: Huathiri mavuno kwa asilimia 80 mpaka asilimia 100%.

4. Kuoza kwa kiazi (Bulb rot): Husababishwa na fangasi. Ugonjwa huu hutokea vitunguu vikishakomaa, huku udongo ukiwa na maji maji.  Vitunguu vikishakomaa visimwagiliwe tena.


Uharibifu wa vitunguu usiotokana na magonjwa1. Kuchipua baada ya kuvunwa: Hali hii hutokea endapo vitunguu vitavunwa kabla ya muda wake.  Endapo vitunguu havitakaushwa vizuri baada ya kuvunwa. Hali hii husababisha uharibifu mpaka asilimia themanini (80%).  Sehemu ya kukaushia vitunguu iwe na hewa inayozunguka na mwanga wa kutosha. Vitunguu vikiwekwa gizani huchipua kwa urahisi.

2. Muozo laini (Soft rot): Ugonjwa huu hushambulia vitunguu baada ya kukomaa; husababishwa na vimelea (bacteria). Vitunguu hutoa harufu mbaya ya uozo.  Kuepuka hilo vuna kwa wakati unaofaa, hifadhi sehemu yenye mwanga na hewa inayozunguka.

Virusi
Unaweza kuzuia vimamba ambao ndio wanaoeneza virusi kwa kutumia dawa za kuulia wadudu.

Vitunguu vinalipa

“Vitunguu vinatofauti kidogo na mazao mengine ya mboga mboga kwa kuwa si rahisi kukosa soko, na endapo bei si nzuri unaweza kuhifadhi kwa muda ili kusubiri bei iwe nzuri.” Ni maneno ya mkulima Peniel Rodrick (pichani) ambaye amejikita zaidi katika kilimo cha vitunguu kibiashara.  Mkulima huyu kutoka kijiji cha Oloigeruno anasema pamoja na kwamba anazalisha pia mazao mengine, lakini ameamua kujikita zaidi kwenye vitunguu baada ya kugundua siri na namna ya kupata faida zaidi.

Toka aanze kilimo cha vitunguu miaka 12 iliyopita, ameweza kuendesha maisha yake vizuri, ikiwa ni pamoja na kuanzisha miradi mingine kama ufugaji wa ng’ombe, kujenga nyumba ya kisasa na kuitunza familia yake ya watoto watatu ipasavyo. Pamoja na hayo anasema tatizo kubwa la vitunguu ni magonjwa na wadudu. Anasema si rahisi sana kugundua mara moja kuwa kuna ugonjwa unaoshambulia vitunguu, na mara unapogundua unakuwa umefikia kwenye hali mbaya.

Kwa maelezo zaidi wasiliana na Bwana Suleiman Mpingama mkufunzi na mtaalamu wa mazao kutoka chuo cha kilimo Tengeru. Unaweza kutumia namba +255 756 428 877.